Pages

Friday, August 5, 2011

MWAKA MMOJA TANGU KIFO CHA EDWIN BEATUS MACHA

KIPINDI HIKI MWAKA JANA
Wazazi wa Edwin Beatus Macha wakiwa SAUT-Mwanza kwa Ajili ya Siku Ya Kumbukumbu ya Mtoto wao Mpendwa

“Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu” (Isaya 55: 8,9). 

Haya ni maneno ambayo Edwin alisema mara nyingi kuwa ndiyo aliyoyapenda sana katika Biblia…! Bado Napata shida kumuelewa.
Edwin Beatus Macha
Nakikumbuka vizuri sana kipindi hiki mwaka jana. Nilikuwa mjini Njombe nikifanya mafunzo yangu kwa vitendo katika Kitengo cha Uchumi na Mipango katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Kilikuwa ni kipindi cha furaha sana kutokana na muunganiko wa karibu na marafiki zangu wakubwa.

Ni kipindi cha siku za mwisho mwisho za rafiki yangu mpendwa duniani, Edwin Beatus Macha. Kilikuwa kipindi ambacho japo kuwa yeye alikuwa Dar es Salaam, tulikuwa tunawasiliana sana hasa kwa ajili ya research zetu, maana tulipanga kuwa tumezimaliza kabla muda wa kufungua chuo kufika. Tulikuwa tumepania sana.

Ninakumbuka mambo mengi sana. Hasa kilipofika kipindi ambacho Edwin anaanza kutafutwa, kuanzia Ijumaa, Agosti 27, 2010. Nilipokea simu ya kwanza toka kwa Rose, akiniuliza eti Edwin yuko wapi? Sikushituka, hata kidogo. Nilicheka sana, maana sikutegemea kuulizwa swali hili, wakati akijua kabisa mimi niko Ludewa (ukweli ni kuwa nilikuwa Njombe, daima rafiki zangu hujua niko Ludewa kwa namna nilivyo na mapenzi nayo) na yeye yuko Dar es Salaam, ingewezekanaje mimi kujua? 

Akanimbia kwa sauti ya kuonesha wasi wasi, “Ed hapatikani kwenye simu zake zote!” Hili pia halikuweza kunishtua. Sikushtuka kwa kuwa nilidhani pengine yuko bize anafanya kitu fulani, alikuwa ana kawaida ya kuzima simu akiwa anafanya kitu muhimu kama kuandika na kama hakutaka kusumbuliwa na watu na anakimbizana na wakati. Ndicho pia nilichomjibu Rose. Atakuwa yuko bize. Aliposema alipaswa kuonana naye siku ile Ubungo, sikushtuka pia, nikahisi labda Rose kamkorofisha hivyo kaamua kwenda ‘offline’! 

Kamwe sikuwaza kuwa kuna uwezekano wa baya lo lote kumfika Edwin, kwa kweli hakukuwa na uwezekano wa kichwa changu kuwa na fikra hizo, hata chembe. Hata aliposema nyumbani pia wanamtafuta, sikupata hofu kwa kuwa kama kazima simu, hakuna awezaye kumpata na kujua aliko hivyo ni wazi nyumbani pia wangemtafuta! Hakukuwa na nafasi kabisa ya kuwaza baya! Zaidi sana kwa kuwa nilikuwa nawafahamu wote wawili vizuri, na namna Rose anavyoongea kwa hisia hata kwenye mambo ya kawaida (Mimi, Edwin na Mnyambudu tuliwahi kumfanya Rose alie sana siku moja, kisa tulimbana kwa hoja juu ya usawa kati ya wanaume na wanawake, lakini kiukweli, tulikuwa tu tunatumia hoja zake mwenyewe kumshinda), kama aliweza kulia kwenye hili, sikuona kabisa hatari katika yeye kuongea kwa unyonge na huzuni kubwa kutika kutokupatikana hewani kwa Edwin. Aliponiambia alidhani yupo kwetu Ludewa, nikacheka sana! Niliona ni mfululizo wa kuwaza yasiyokuwepo ambayo ni kawaida kwa watu wanaoendeshwa kwa hisia. 

Punde baada ya kuongea na Rose, simu yangu ikaita, Raymond Massawe, nikaipokea kama nifanyavyo siku zote, tukaongea na kujadili suala la Edwin. Yeye pia aliniambia kuhusu Edwin, alinieleza kwa kirefu kuhusu mashaka yalivyotanda miongoni mwa familia na rafiki zake. Lakini bado tulikuwa chanya sana, tulifikiri pia pengine kaamua kufanya hivyo makusudi. Pia, siku za karibuni, alikuwa na mahusiano ya karibu sana na mtu mmoja (sitamtaja) ambaye tunajua kuwa ni mtu mkubwa katika kitengo nyeti cha usalama hapa nchini, tuliwaza pia pengine kuwa inawezekana ameingia katika mlengo huu wa maisha. Kweli, baada ya kuongea na Raymond, nilipata hofu kuu, ila sio hofu ya kifo. Hofu ya kwa nini Edwin ameamua kufanya hivi? Na tulikuwa na mipango mingi pamoja, je, itafanikiwa kama kaamua kuishi maisha ya mtindo huu? Sikuwaza kabisa juu ya hofu ya mauti. Haikuwa na nafasi kichwani mwangu. Baada ya hapo nilipokea simu nyingi toka kwa watu mbalimbali, na wengine nilikuwa hata sifahamiani nao vizuri, na wengine siwafahamu kabisa. Niliongea pia na Gillian, ambaye alikuwa na hofu ya hali ya juu. Ilikuwa ni kipindi kigumu, chenye mashaka mengi. Kiubaridi cha hofu kikaanza kunipata. 

Nilipoambiwa kuwa Edwin anatafutwa hadi hospitalini na kwenye vituo vya polisi, nilianza kuingia shaka zaidi. Lakini nikafikiri pia, kuwa kutokana na kutokujua alipo, na upendo mkubwa wa familia, ilikuwa ni namna pekee ya kutenda.

Nilipoambiwa amepatikana, nilifurahi sana, lakini baada ya kuelezwa namna alivyopatikana, na hali yake illivyokuwa, moyo wangu ulipondeka kabisa. Sikuweza kuendelea na nilichokuwa nakifanya wakati ule, nikarejea nyumbani. Wakati nikiongea na baba yangu, kuwa Edwin kapatikana, na yuko ICU, kama wengine wote, alisema tuwe na imani, tuwe na moyo mkuu, tuwe na matumaini na tumuombee ili aweze kupata nafuu na kupona kabisa.

Nilikuwa nafuatilia kwa karibu kwa simu maendeleo yake. Ndipo ilipofika siku ile, siku ambayo sitaisahau maishani mwangu Jumatatu, Agosti 30, 2010. 

Nilikuwa ofisini toka asubuhi, lakini uwanja wa Saba Saba, karibu tu na makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, kulikuwa kuna uzinduzi wa gazeti moja. Mrisho Mpoto pia alikuwepo. Kwa kuwa moja ya mipango yetu ilikuwa ni kutafuta magazeti ya kuandikia, nikaona ni vema niende nikawasikilize. Kabla hata uzinduzi wenyewe haujafanyika, simu yangu ikaita, Raymond Massawe, sijui kwa nini, lakini sikuipenda simu hii. Hata sikuweza kuipokea pale nilipokuwa nimesimama. Badala yake, nikaanza kutembea kwa kasi kuelekea nyumbani, ndipo nilipopokea simu ile. Sauti yake tu, iliongea yote. The worst had happened. "Vumbi Vumbi!" kama yeye mwenyewe alivyopenda kusema pale mambo yalipokuwa yanakwenda mrama! VUMBI VUMBI!

Badala ya kwenda nyumbani, nikajikuta nimeenda ofisini kwa baba yangu. Sikupata nafasi ya kumueleza, nikapitiliza hadi stendi na kufanya booking kwa ajili ya safari ya Dar es Salaam. Nawashukuru sana wazazi wangu maana walielewa na kuuchukulia msiba huu kama wao, na kunisaidia mpango wote wa safari.
Katika kipindi hiki chote, ilikuwa vigumu sana kuwasiliana uhalisia wa hali ya Edwin hasa kwa Gillian Mombo. Nilkuwa najua wazi kuwa itafikia wakati ataujua ukweli, sio kwa sababu mtu angemweleza, bali kwa kuwa kila aliyekuwa anamuuliza, badala ya kusema alikuwa anaendelea vizuri kama ilivyokuwa zamani, ikawa hajui anaendeleaje, sijawasiliana nao hivi punde na kadhalika.
Niliwaza kuhusu familia yake, mama, baba, wadogo zake, ndugu na majirani. Kama mimi rafiki nimeguswa hivi, itakuwaje kwa watu hawa? Nilitamani hili lisiwe kweli, lakini dunia hii inaendeshwa kwa namna yake, na Edwin ndio akawa kamaliza safari yake ya hapa duniani, katika namna isiyokuwa ya kawaida.

 KIFO CHA EDWIN BEATUS MACHA
Kulikuwa na nadharia nyingi ambazo zilitawala katika kipindi hiki kuhusiana na namna mauti yalivyomfika Edwin. Kifo hiki kiligubikwa na utata mkubwa, na uzushi mwingi sana.

Edwin katika Moja ya Picha alizotengeneza mwenyewe enzi za uhai wake

Edwin alikuwa anakaa kwa baba yake mdogo, Dar es Salaam, siku hiyo alitumwa na mama yake mdogo akachukue kiasi cha pesa ATM, apeleke kiasi fulani cha pesa hizo kwa baba yake mdogo huyo, ambaye anafanya kazi ofisi ya Takwimu, Posta. Baada ya kupeleka pesa kwa baba yake mdogo, ndipo alipoelekea eneo la kituo cha basi, maeneo ya karibu tu na Billcanas, ndipo alipovamiwa na vibaka, waliojifanya kumfananisha na mwizi aliyeiba vifaa vya magari katika eneo hilo hilo wiki mbili zilizopita. Mtindo wa kuwaibia watu kwa kuwasingizia ulikuwa umepamba moto hasa katika kipindi hiki jijini Dar es Salaam. Walimuibia pesa zote zilizobakia, pamoja na simu zake mbili. 

Kadiri ya mashuhuda,(kuna shuhuda mmoja ambaye anakaa karibu kabisa na Baba yake mdogo na Edwin, lakini kutokana na maisha ya Dar, kila mtu na maisha yake, hivyo hakumtambua kabisa kwa wakati huo) wezi hao walimpiga mtama, wakamuibia na wala hawakumpiga sana. Baada ya tukio hilo, Edwin aliinuka, akakaa chini kajiinamia.

Ndipo polisi walipofika na kumchukua Edwin, AKITEMBEA KWA MIGUU YAKE!, na kumpeleka katika hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu ya vidonda vidogo vidogo (kadiri ya daktari aliyemhudumia ‘minor injuries’). Na kwa kuwa hakuumia sana, daktari aliyemhudumia akamruhusu kurudi kituoni, ambako alilala.

Polisi walimbambika kesi Edwin, ya wizi wa laptop. Wakampigia mtu mmoja wa Tegeta, ambaye alikuwa kaibiwa laptop siku za nyuma, na kumtaarifu kuwa wamempata mwizi wake. Habari hizi zilikuja kujulikana baada ya shemeji ya mtu huyu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa CA-SAUT, ambaye pia alikuwa ni mpenzi wa rafiki mmoja wapo wa Edwin anayesoma SAUT pia (sitawataja) alipomweleza mpenzi wake huyu, naye akaweka hili bayana. Bahati mbaya binti huyu hakuwa na uwezo wa kutoa ushahidi kwa kuwa ilikuwa ni kumsaliti shemejiye, ambako ndiko alikuwa anakaa…! Na dada yake pia! Hivyo hata tulipojaribu kutafuta namna nzuri ya kupata ushahidi wake, aliingiwa na hofu, tulijaribu kumtumia dada mmoja, Abela, ambaye alikuwa anasoma darasa moja na Edwin, akampigigia simu, wakapanga kukutana, lakini baaday akafunga simu yake. Nilikuwa pamoja na Abela na Benson muda mwingi tukisubiri labda atapatikana kwenye simu lakini hakupatikana. Bahati mbaya zaidi, mpenzi wake pia akaingiwa na hofu, hivyo akawa anaogopa kutupeleka kwao…! (Siwalaumu hata chembe).

Lakini alichokisema mdada huyu ni hiki: Shemeji yake aliitwa asubuhi ya jumamosi, akamuone mwizi wake, ndipo alipooneshwa Edwin. Wakamhoji na Edwin alikiri, na aliwaambi laptop iko nyumbani, waende tu nyumbani naye atawapa. Na aliwaambia kuwa anazo mbili! (Ni kweli kulikuwa kuna laptops mbili nyumbani, moja yake na nyingine ya Baba yake mdogo!) Na Edwin aliandika maelezo ya kukiri kosa hilo. Maelezo hayo hayakuweza kupatikana tena baada ya taswira ya undani wa kifo cha Edwin kuanza kujidhihirisha.

Hawakumpeleka nyumbani, wala hawakumtaarifu ndugu ye yote, wala kupiga simu chuoni (maana alikuwa anakitambulisho cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT)). 

Cha ajabu, Edwin alipelekwa Hospitali ya Rufaa Muhimbili akiwa mahututi. Na inaonekana alipelekwa baada ya baba yake mdogo kufika kituoni hapo. 

Kadiri ya baba yake mdogo; alipitia vituo vingi na hospitali nyingi ndipo alipofika hospitali ya Mnazi Mmoja. Hapo ndipo akaambiwa kuwa kuna mgonjwa alitibiwa hapo wa namna anayomuelezea, lakini alirudishwa kituoni. Alipofika kituoni, alizungushwa sana, aliambiwa asubiri kwa zaidi ya saa moja! Alifika Kito cha Polisi Kati mnamo saa kumi jioni, ndipo alipoanza kuzungushwa….! EDWIN ALIPOKELEWA HOSPITALI YA MUHIMBILI SIKU HIYO HIYO MNAMO SAA KUMI NA MOJA ZA JIONI! AKIWA NA MAJERAHA MAKUBWA KICHWANI….NA ALIYEPOTEZA FAHAMU! 

Alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, ambaka alikaa mpaka mauti yalipomfika Jumatatu Agosti 30, 2011. Ufuatiliaji polisi ukaleta utata zaidi. Mpaka Alhamisi, kulikuwa hakuna jibu lo lote la kueleweka kuhusiana na mazingira ya kifo cha Edwin kutoka polisi. 

Mzee Beatus Macha, baba yake Edwin aliweka wazi msimamo wake. Hakutaka kumshtaki wala kumuharibia ye yote nafasi yake, alitaka tu ukweli juu ya kifo cha mwanaye. Alitaka kupata majibu ya maswali mengi magumu na tata yaliyotokana na mazingira ya kifo cha mwanaye. Lakini kutokana na mfumo wan chi hii, ikagonga mwamba. Hata baada ya kupata fursa ya kuonana na Kamanda wa Polisi Mkoa, bado majibu yake hayakuweza kukidhi kabisa haja ya moyo wa wazazi na marafiki kutaka kujua ukweli wa kifo cha mpendwa wao.

UTATA! UTATA! UTATA!
Utata mkubwa ulikuwa wazi hasa katika maneneo yafuatayo kama yalivyoanishwa kwenye Utata wa kifo cha Edwin Macha, Mwanafunzi wa St. Augustine, Tanzania, • Posted by GLOBAL on September 15, 2010 at 5:30pm
1.kama alipigwa na wananchi, inamaana wananchi wanashabaha sana mpaka wote wampige sehem moja tu? because aliumia sehem ya kichwani....
2.watu waliokuwepo sehem ya tukio walipohojiwa, walikiri kwamba alichukuliwa na polisi akiwa mzima na anatembea mwenyew wakampeleka kituon
3. daktari wa mnazi mmoja alipohojiwa, alisema, marehem hakuwa na kidonda mwilini pake zaidi ya michubuko midogomidogo ndo maana alimpa pain killers tu...na akamruhusu
4.kama marehem alipigwa na wananchi mpaka akapoteza faham, siku ya ijumaa ilikuwaje akapelekwa kulala kituon? pia, information zake walizipataje? hata kama walitumia ID ya chuo, makazi yake na umri wake waliujuaje?
5.kama walitumia kitambulisho cha chuo kwa nini hawakutoa taarifa SAUT mpaka sisi tulipompata siku ya jumamosi jion ndo baadae wakajifanya kupiga simu SAUT?
6. kuna kesi kibao walimbambikia, km, wizi wa laptop, wizi wa kutumia silaha, kutaka kuiba gari, etc na wakajifanya kuweka na walalamikaji, mbona walalamikaji walikana?
7. marehem alikuwa hajapewa chakula tokea ijumaa hadi siku ya jumamosi tulipompata, na kuna polisi walikiri kwa hilo, je polisi wanawez kusema ni kwanini?
8.polisi walitusumbua sana kutoa kibali cha marehem kufanya postmortem... na hata waliporuhusu,.. wakakataa kusain report ya postmortem kutoka kwa dactari that day... tukazidi kujiuliza kwanini...
9. polisi wanasema alipigwa jumamosi, ilikuwaje alipelekwa dispensary ya mnazi mmoja siku ya ijumaa akiwa na pingu na escot ya polisi? au siku hizi mtu anatibiwa ndo anaugua?

Pia vyombo vya habari vilichangia kupotosha ukweli wa tukio zima. Ikumbukwe kwamba, kipindi hiki kilikuwa cha kampeni za uchaguzi mkuu, hivyo habari wala haikuwa na mvuto kwa vyombo vingi vya habari vilivyokuwa vimeelekeza macho yao yote kwenye kampeni ya uchaguzi, CHADEMA Vs CCM, huku mpiganaji wa ukweli akipotea kimya kimya.

Kulikuwa na ufuatiliaji mwingi, mpaka mwisho mwishoni, ikatumika busara ya hali ya juu kabisa. Mpendwa wetu amekwisha tutoka. Yote yaliyotokea, hayawezi kurekebishwa, maji yalikwisha mwagika, na mpendwa wetu aliendelea tu kusota mochwari. Sio kitu kizuri kwa tamaduni za kiafrika kuacha mpendwa wetu hajazikwa. Hivyo ikaamuliwa azikwe. Post-mortem ilikuwa ya utata pia, wazazi walitaka uchunguzi binafsi, lakini uliofanyika ni wa kipolisi tu, ambao hakuna ndugu aliyeruhusiwa kushuhudia, zaidi ya kuruhusiwa kutambua mwili wa marehemu tu.

Mimi na baba yake mdogo ndio tuliingia kuutuambua mwili wa Edwin. Sitasahau, kumuona Edwin kalazwa pale. Alionekana kuvimba usoni, na alikuwa mweusi sana. Sikuweza kuona sana kwa kuwa alikuwa amelazwa chali. Na baada tu ya kusema ndiye, tukaamuriwa kutoka nje. Ni mandhari ambayo haitapotea kichwani mwangu. Edwin niliyemjua mimi, kumuona katika hali ile…! 

Basi, taratibu za safari zikapamba moto. Misa ya kumuaga ilifanyika Kanisa la Muhimbili, ibada ikiongozwa na Dk. Fr. Matumaini, Mkurugenzi wa tawi la SAUT la Msimbazi. baada ya ibada na kuagwa na wanafunzi wengi aliosoma nao tokea shule ya msingi, sekondari na chuo kikuu. Ulikuwa ni misiba mkubwa sana. Na baada ya taratibu zote za kutoa heshima ya mwisho, safari ya kuelekea Moshi ikaanza.

EDWIN KWAO MOSHI
Mwili wa Edwin Beatus Macha Ukifikshwa Nyumbani Kwao- Moshi
Tulifika Himo usiku wa manane. Tukasimama na kusubiri mapambazuko na kuelekea kijijini kwa akina Edwin, Kirua Vunjo. Tulipokelewa na watu wengi wenye huzuni kuu. Wanaume, wanawake na watoto wengi walikuja kumlilia mpendwa wao. Watu walikuwa wamejawa na huzuni pia ghadhabu kutokana na namna Edwin alivyofikwa na mauti.
Ibada ya mazishi ilifanyika nyumbani kwao, na alizikwa umbali mdogo karibu na nyumbani kwao. Watu walihuzunika na kughadhabika zaidi wakati Mzee Beatus Macha alipokuwa anaelezea namna ambavyo mauti yalimfika mwanaye.
Edwin Beatus Macha alikuwa kipenzi cha watu wote waliopata kumjua. Hivyo huzuni ilikuwa kubwa katika watu wote wa eneo lake, na marafiki zake wote nje na ndani ya nchi.
Jeneza lenye Mwili wa Edwin likiwa Kaburini
Kaburi la Edwin lilipambwa sana. Lilikuwa na maua na mishumaa mingi. Alfajiri baada ya kuzikwa kwake, nilienda, peke yangu kwenye kaburi lake. Nilikuta mshumaa mmoja ungali ukiwaka. Nikaiwasha na mingine iliyobakia, nilikaa kitambo, nikatafakari mambo mengi, na ilikuwa fursa kwangu kumuaga kwa mara nyingine rafiki yangu mpendwa.
Wazazi na Baadhi ya Marafiki na Ndugu Waliohudhuria Mazishi ya Edwin - Moshi


KIFO CHA EDWIN NI KAMA YA YESU MSALABANI
Katika imani ya kikristo, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na Mungu, alisulubishwa msalabani. Hii ilikuwa ni adhabu kwa ajili ya wanyang’anyi na wahalifu wengine. Yesu, alitolewa afe kwa aibu kuu, ilhali hakustahili. Vivyo hivyo Edwin, amekufa kifo cha aibu, asichokistahili, lakini kilichotuachia fundisho kubwa.

KUMBUKUMBU ISIYOFUTIKA
Edwin ameendelea kukumbukwa na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zake wakati wote. Jumuiya ya Wanafunzi wa Uchumi SAUT walioandaa siku maalum ya kumuenzi, Novemba 20, 2010. Wazazi wake pamoja na mama yake mdogo walihudhuria. Baba yake alielezea tena kwa uchungu namna mwanaye alivyofikwa na mauti, sehemu ya maelezo yake ndiyo hasa ni msingi wa maelezo yaliyotelewa nami humu. Kweli kuna mambo mengi sana ambayo yalizunguka maisha na mauti ya Edwin, sio rahisi kuyaelezea yote namna inavyopaswa.
Pia siku kuzaliwa kwake, Februari 19, iliadhimishwa misa maalum katika Kanisa Katoliki – Malimbe (SAUT) kwa ajili ya kumuombea.
Baadhi ya Marafiki waliohudhuri Siku ya Kumbukumbu Novemba 20, 2010 -SAUT
Yako mengi sana ambayo hayaandikwa kuhusu kifo cha Edwin. Marafiki zake wote toka enzi za utoto, shule ya msingi, sekondari na chuo, wana mengi ya kumuelezea. Nawakumbuka sana namna walivyoshiriki katika msiba mzima. Walionesha upendo wa hali ya juu…natamani ningeweza kuwataja wote lakini sitaweza kuwamaliza!
Baadhi ya Marafiki Baada ya Mazishi - Moshi
Wengi watembelea akaunti yake ya Facebook http://www.facebook.com/profile.php?id=557966030 na pia ALWAYS IN OUR HEARTS EDWIN BEATUS MACHA
Baadhi ya Wapiganaji katika Kipindi Kigumu Cha Msiba
 
Tuendelee kupeana moyo na nguvu, kufarijiana na kuwasha matumaini katika kumuenzi mwenzetu. UPENDO WAKE KWETU DAIMA NI MKUU KULIKO MAJONZI YALIYOTUFIKA!

Wednesday, August 3, 2011

KIPINDI HIKI MWAKA JANA...!

Nakikumbuka kipindi hiki kwa namna ya pekee...! Ni kipindi cha siku za mwisho za mpendwa wetu hapa duniani. Daima nimekuwa namkumbuka, ili kipindi hiki nimekuwa na mengi ya kutafakari.
Daima nitamkumbuka Edwin!